MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI, MECHI SEPT 26
Mtihani wa uwakala wa wachezaji (players agent) na
uwakala wa mechi (match agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) utafanyika Alhamisi ya Septemba 26 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi kwenye
ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kutakuwa na jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15
yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za kimataifa za mpira wa miguu na matano
yatatoka TFF kuhusiana na kanuni mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini.
Kwa ambao wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa
katika lugha ya Kiingereza ambayo ni moja kati ya lugha nne rasmi za FIFA
wanatakiwa kujisajili TFF kwa ada ya dola 50 za Marekani ambapo watapewa
utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga.
Mtihani huo
utafanyika saa 4 kamili asubuhi, na muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika
90.
Mpaka sasa Tanzania ina mawakala watano wa wachezaji
wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally
Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.
WAAMUZI VPL KUFANYA MTIHANI WA UTIMAMU WA
MWILI
Waamuzi
wote wa daraja la kwanza (Class I) wanaotaka kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu wa 2013/2014 wanatakiwa kuhudhuria mtihani wa utimamu wa mwili
(physical fitness test) utakaofanyika katika vituo viwili.
Mtihani
huo utafanyika Agosti 12,13 na14 mwaka huu katika vituo vya Dar es Salaam na
Morogoro. Kituo cha Mwanza kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Geita, Kagera,
Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.
Kituo cha Dar es
Salaam kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma,
Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na
Tanga.
Washiriki
wote wanakumbushwa kuwa ni lazima wafuate utaratibu huo wa vituo, na si
vinginevyo. Pia waamuzi waliofungiwa (sio maisha) wanatakiwa kushiriki katika
mtihani huo.
RATIBA LIGI
DARAJA LA KWANZA AGOSTI 14
Ratiba ya Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2013/2014 inayoshirikisha timu 24 zilizo katika
makundi matatu zikicheza kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) inatarajiwa
kutolewa Agosti 14 mwaka huu.
Kundi A linaundwa
na timu za Burkina Moro ya Morogoro, JKT Mlale (Ruvuma), Kimondo SC (Mbeya),
Kurugenzi Mufindi (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro),
Polisi (Iringa) na Polisi (Morogoro).
African Lyon (Dar
es Salaam), Friends Rangers (Dar es Salaam), Green Warriors (Dar es Salaam),
Ndanda (Mtwara), Polisi (Dar es Salaam), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp
(Dar es Salaam) na Villa Squad (Dar es Salaam) zinaunda kundi B.
Timu za kundi C ni
JKT Kanembwa (Kigoma), Mwadui (Shinyanga), Pamba (Mwanza), Polisi (Dodoma),
Polisi (Mara), Polisi (Tabora), Stand United (Shinyanga) na Toto Africans
(Mwanza).
Tunapenda
kukumbusha kuwa dirisha la usajili kwa madaraja yote ni moja ambapo usajili wa
hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 3 mwaka huu wakati hatua ya pili
ni Agosti 14 hadi 29 mwaka huu. Dirisha dogo litafunguliwa Novemba 15 hadi
Desemba 15 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)