Tuesday, June 14, 2011






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAREHE 14 JUNI 2011UFAFANUZI KUHUSU UCHAGUZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB (VILLA) NA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF 1.

UTANGULIZI

Hivi karibuni kumekuwa na maelezo mbalimbali katika vyombo vya habari kuhusu uchaguzi wa Klabu ya Villa na wanachama wengine wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu uchaguzi huo na chaguzi nyingine za wanachama wa TFF.


Kila mwombaji uanachama wa TFF hana budi kutimiza masharti yalivyoainishwa kwenye Katiba ya TFF ili kuwa mwanachama wa TFF. Kati ya masharti hayo ni Tamko la kimaandishi kuwa anakubali kufuata Katiba ya TFF, Kanuni na maagizo katika muundo wake wa sasa na mabadiliko ya baadae na maamuzi ya FIFA, CAF, CECAFA, TFF na vyombo vyake (Ibara ya 7(2)(c) na Tamko kwamba atahakikisha kwamba Katiba ya TFF inaheshimiwa na wanachama wake na mtu yeyote mwenye mahusiano naye (Ibara ya 7(2)

Baada ya kutimiza masharti yote ya maombi ya kuwa mwanachama, kila mwanachama wa TFF anawajibika, pamoja na kutimiza masharti na matakwa mengine ya kikatiba


Kuwa mwaminifu na mtiifu kwa TFF kwa maana ya kutofanya vitendo vinavyokwenda kinyume na matakwa ya TFF kama ilivyoanishwa kwenye Ibara ya 12 (1) (b).


Kufuata Katiba, kanuni, maagizo na maamuzi ya FIFA, CAF, CECAFA na TFF. (Ibara ya12 (1) (d)).


Kutokuwa na uhusiano wowote wa kimichezo na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa. (Ibara ya12 (1) (k))


Kutimiza wajibu wowote unaotokana na Katiba, Kanuni, maagizo na maamuzi ya TFF. (Ibara ya12 (1) (n))


Kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama ya kawaida ya Sheria. (Ibara ya12 (2) (e)).

Mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa viongozi wa TFF na wa wanachama wote wa TFF yamekasimiwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49 (1)

Kanuni za Uchaguzi za TFF na wanachama wake zimetungwa na kuidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 34(k)

2.MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB Klabu ya Villa ni mwanachama wa TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 5 (3) na 6(5).


Katiba ya Villa Ibara ya 1 (6) inatambua Mamlaka ya TFF. Ibara hiyo inasomeka hivi: “Klabu ya mpira wa miguu ya Villa Squad ni mwanachama wa TFF, itaheshimu katiba, kanuni, maagizo na maamuzi ya TFF na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake”.


Pamoja na matakwa hayo hapo juu, Katiba ya Villa katika kuzingatia uanachama wa Villa kwa TFF inazingatia pamoja na matakwa mengine haya yafuatayo kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Villa:

bara ya 11: Wajibu wa wanachama wa Villa; Kila mwanachama wa Klabu ya Mpira wa miguu ya Villa Squad atakuwa na wajibu ufuatao zaidi ya ule uliotajwa kwenye Kanuni za Asasi: Ibara ya 11 (1) (c): Kukubali kufuata Katiba hii, kanuni, maagizo na maamuzi ya Klabu ya miguu ya Villa Squad na TFF. (Ibara ya 11 (2) (b)): Kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama ya kawaida ya Sheria.


Ibara ya 25:Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya Klabu ya mpira wa miguu ya Villa Squad hana budi kutimiza masharti yafuatayo: 1. Awe na uzoefu wa uendeshaji mpira wa miguu uliothibitishwa.2. Asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo bila ya kupewa uchaguzi wa kulipa faini.3. Awe na umri angalau kuanzia miaka 18.4. Awe anajua kusoma na kuandika na awe na elimu ya msingi hadi sekondari.5. Awe na cheti cha elimu ya msingi na sekondari.

Katiba ya Villa, kama zilivyo katiba za wanachama wa TFF inatambua mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Ibara ya 40(5) ya Katiba ya Villa inasomeka: Kamati hii itafanya kazi chini ya kamati ya uchaguzi ya TFF.

Kwa kuzingatia wajibu wake wa kikatiba kama ilivyoainishwa hapo juu, TFF iliiagiza Klabu ya Villa kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Klabu ya Villa kuanzai tarehe 02 Mei 2011 kwa barua yenye Kumbukumbu Na. TFF/ADM/EC11./09 ya tarehe 30 Aprili 2011 na pia kuagiza kuwa uchaguzi huo ufanyike kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na ukamilike kabla ya tarehe 20 Juni 2011.:

Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Villa kukamilisha zoezi la usaili, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa barua yenye kumbukumbu Na. TFF/ADM/EC.11/17 ya tarehe 06 Juni 2011 iliiomba Kamati ya Uchaguzi ya Villa kuwasilisha taarifa ya mchakato wa uchaguzi, ikitimiza majukumu yake ya kikatiba na kikanuni ya kutathmini na kusimamia uchaguzi wa wanachama wa TFF.

Baada ya kupata taarifa kutoka Kamati ya Uchaguzi ya Villa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilifanya kikao na Kamati ya Uchaguzi ya Villa katika makao makuu ya Klabu ya Villa hapo tarehe 08 Juni 2011, ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu uzingatiaji wa Kanuni za Uchaguzi na kujadili matayarisho ya uchaguzi ili kuhakikisha kama mahitaji yote ya kufanikisha uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 12 Juni 2011 yamekamilika.

Kwa kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikuridhika na maelezo yaliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya Villa kuhusu matokeo ya usaili wa wagombea na vielelezo vilivyotajwa na Kamati Uchaguzi ya Villa kuwapitisha baadhi ya wagombea uongozi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa barua yenye kumbukumbu Na. TFF/ADM/EC.11/18 ya tarehe 09 Juni 2011 iliiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa uwasilishe TFF nakala za fomu za kuomba uongozi za waombaji uongozi wote waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Villa, zikiwa zimeambatanishwa na nakala za uthibitisho wa sifa za wagombea uongozi, kwa mujibu wa Ibara ya 10 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliagiza kufanyika hivyo kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26 (2) inayoipa mamlaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuingilia mchakato wa uchaguzi wa wanachama wa TFF wakati wowote ule kuangalia na kuthibitisha usahihi wa mchakato, kuhakiki na kujiridhisha kwamba Kanuni za Uchaguzi, matakwa ya Katiba ya mwanachama wa TFF, Katiba ya TFF na FIFA yanazingatiwa.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF, katika kikao chake kilichofanyika tarehe 10 Juni 2011 kupitia fomu za maelezo ya wagombea uongozi wa Klabu ya Villa na nyaraka za uthibitisho wa sifa za wagombea uongozi, ilibaini kuwa wagombeaBw. Mohamed Kea Mohamed, Bw. Ramadhani Soud Iddi, Bw. Alwan Mohamed Geyash, Bw. Ali Mohamed Daddy Baucha, Bw. Ally Ahamed Mpemba Bw. Said Yusuf Chacha, Bw. Idd Mohamed Mbonde na Bw. Abdalla D. Majurah hawakidhi sifa za wagombea uongozi kama zilivyoainishwa kwenye ibara ya 25 (5) ya Katiba ya Klabu ya Villa. Kwa kutotimiza masharti na sifa za uongozi kwa mujibu wa Katiba ya Villa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaondoa katika orodha ya wagombea uongozi kwa nafasi walizoomba kugombea. Kamati ya Uchaguzi ya Villa ilitaarifiwa maamuzi hayo ya Kamati na kuagiza uchaguzi wa Klabu ya Villa Squad utafanyika kama ulivyopangwa tarehe 12 Juni 2011, kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na kwamba nafasi ya Mwenyekiti haina mgombea na itajazwa baadaye kwa mujibu wa Katiba ya Klabu ya Villa Squad Ibara ya 28(c), yaani kwenye uchaguzi mdogo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka uonaofuata baada ya uchaguzi. Kamati ya Uchaguzi ya Villa ilitakiwa kwa barua ya TFF yenye kumbukumbu EC/TFF/06/2011/002 ya 10 Juni 2011kutekel

za maamuzi hayo ya TFF.

3. KUTOFANYIKA UCHAGUZI WA VILLA

Kutofanyika kwa uchaguzi wa Villa ni ukiukwaji wa maagizo na maamuzi ya TFF na ukiukwaji wa Katiba ya Villa na TFF.

Kuahirisha uchaguzi wa Villa kulikofanywa na mkutano mkuu wa Villa ni kukiuka Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10 (6) inayokataza kubadili tarehe ya uchaguzi au kufuta uchaguzi ambao umekwisha tangazwa na Kamati ya Uchaguzi bila idhini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Kutoiruhusu Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kukiuka matakwa ya Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) inayoipa mamlaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF.

4. KUBADILI KATIBA BILA IDHINI YA TFF

Kitendo cha kubadili Katiba ya Villa katika mkutano mkuu wa uchaguzi ni kukiuka Katiba ya TFF Ibara ya 12 (1)(b) na (c).

Kubadili vifungu vya Katiba ya Villa na kuweka vipengele vinavokinzana na Katiba ya TFF ni kukiuka Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 6(a) na (b) na Katiba ya TFF ya 12 (1) (d) na (e). Mabadiliko ya Katiba ya Villa yaliyofanywa na tarehe 12 Juni 2011 hayatatambulika na TFF.

5. KUFANYIKA KWA UCHAGUZI WA VILLA ULIOAHIRISHWA KIMAKOSA. TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kutoendelea na vitendo vya ukiukwaji wa Kanuni za uchaguzi.

TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kutekeleza maagizo na maamuzi ya TFF mapema iwezekanavyo kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi kama ilivyoelekezwa na TFF.

TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kuhakikisha kuwa inakamilisha mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na kupata viongozi kabla ya Kikao kijacho cha Kamati ya mashindano ya TFF ambacho kitafanya maamuzi stahiki ya ushiriki wa Klabu ya Villa katika Ligi kuu, endapo Klabu ya Villa haitatekeleza majukmu yake ya kikatiba kwa taratibu zilizowekwa na TFF.

Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa wanaagizwa kutekeleza maagizo hayo hapo juu ili kuepuka hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao na Klabu ya Villa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF na Katiba ya TFF, CECAFA, CAF na FIFA, endapo hawatatekeleza maamuzi ya TFF. 6.

UCHAGUZI WA VIONGOZI WA WANACHAMA WA TFF

TFF inasisitiza kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaendelea na majukumu yake ya kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF na inawataka wanachama wote wa TFF kuendelea kuzingatia Katiba (zinazoendana na Katiba ya TFF) na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na za TFF katika michakato ya uchaguzi wa viongozi wao.

No comments:

Post a Comment